728x90 AdSpace

MPYA

[recent][ticker2]
14 July 2012

Aliyemteka Dk Ulimboka akamatwa

RAIA wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amekamatwa na polisi jijini Dar es Salaam na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumteka na kufanya jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka na .Mtuhumiwa huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema anaitwa Joshua Mahindi 31 na mkazi wa Namanga nchini Kenya

Wakili Komanya alimsomea mashtaka mawili ambapo mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders Club, jijini Dar es Salaam alimteka Dk Ulimboka.nashtaka la pili alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi na Hakimu Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5,2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Taarifa ya Polisi inaonesha kwamba, mshtakiwa huyo anajulikana kwa jina la Joshua Muhindi (31), mkazi wa Namanga nchini Kenya. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa Juni 29 mwaka huu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe baada ya taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Alisema raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938 kilichotolewa Oktoba 11, 2010 katika Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia anamiliki hati ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa Juni 14, mwaka huu Namanga Kenya.

Kwa mujibu wa Kova, baada ya kuhojiwa na polisi, raia huyo alisema alikuja nchini Juni 23, mwaka huu kwa ajili ya kufanya tukio lililotokea Juni 25 mwaka huu na kwamba alijulishwa kuwa yeye na wenzake 12 ndiyo walipangwa kutekeleza tukio hilo.

Alisema raia huyo na wenzake walikuja nchini kwa ajili ya kumdhuru Dk Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina ambaye anaamini ni mtumishi wa Serikali.

 “Baada ya kuhojiwa alidai kuwa yeye ndiye aliyehusika kumteka Dk Ulimboka na wenzake na baada ya utekaji huo wenzake waliondoka,” alisema Kova na kuongeza:

“Alisema walikuja kutekeleza tukio hilo kwa lengo la kujua ni nani anayemshawishi Dk Ulimboka na alipelekwa na mwenyeji wake asiyemtambua hadi katika hoteli moja katikati ya jiji.”

Alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho kama Gun Star chenye makao yake Iwiru Wilaya ya Thika nchini Kenya na kwamba kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer akisaidiwa na Paft.

Alisema pia, mtuhumiwa huyo alidai kuwa, wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini Kenya.

Alisema baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana na kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Gwajima, lakini hakufanikiwa badala yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa Kiriba.

“Alipoonana naye alimweleza kuwa yeye ni mwanachama wa Kikundi cha ‘Umafia’ na kwamba hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu Kenya na nje ya mipaka,” Kamanda Kova alisema.

“Alikwenda katika kanisa hilo kwa ajili ya kufanya toba maana aliona alifanya kitendo cha kinyama hivyo aliona arudi ili akapate toba,” alisema.

Alisema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi  kwa ajili ya kuwatafuta watu wengine waliohusika na utekaji huo.

credit; 
 mwananchi.co.tz

©2012 Nolniz Blog™
Aliyemteka Dk Ulimboka akamatwa Reviewed by Nolniz on Saturday, July 14, 2012 Rating: 5 RAIA wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amekamatwa na polisi jijini Dar es Salaam na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumteka na kufanya jari...

[Breaking News][carousel1]

No comments: